Thursday, November 22, 2012

TAWLAE YAFIKISHA WANACHAMA ZAIDI YA 600.



 
CHAMA cha wanawake wataalamu wa kilimo na mazingira, (TAWLAE), kimefanikiwa katika majukumu yao ambapo sasa kimefikia hatua ya kuwa na wanachama zaidi ya 600 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani.

Akitoa taarifa yake kwenye mkutano wa chama hicho wa kumi na sita mkoani Tabora, Sophia Mlote, alisema kilisajiliwa rasmi mwaka 1995 kikiwa na wanachama 50 wenye fani mbalimbali zikiwemo Kilimo, Mifugo, Mazingira na Maliasili.

Alisema chama hiki kimekuwa na shughuli nyingi za kimaendeleo ikiwemo kumwendeleza mwanamke mtaalam katika sekta ya kilimo, mifugo, maliasili na mazingira.

Mlote alisema kuwa chama hicho pia kimeazimia kukomesha tabia ya jamii kadhaa kutumikisha watoto mashambani na badala yake waende shule wakasome kwani elimu ni msingi wa maisha yao ya baadaye.

Aidha Mlote aliongeza kuwa majukumu mengine ya chama ni kuhamasisha na kuboresha kilimo cha mazao kama mihogo, viazi vitamu na mboga mboga pamoja na usindikaji na uhifadhi wa mazao hayo.

“Hizi sekta ni muhimu kwa maisha ya kila siku ya mwanadamu na hasa akina mama kwani huingiliana na mazingira haya kila aamkapo.....kipekee chama hiki kinashughulika na kuhifadhi mazingira kwa kupanda miti na kuhifadhi mikoko katika ukanda wa pwani”. Alisema Mlote.
 
Akizungumzia baadhi ya kazi za chama hicho alisema kazi nyingine ni kuboresha mifugo wakiwemo kuku wa kienyeji ili kuongeza lishe na kipato katika ngazi ya kaya,kutoa ushauri nasaha kwa wasichana kuhusu elimu ya uzazi na maambukizi ya ukimwi na kusimamia haki na sera ya wazee.

Aliongeza kazi nyingine ni kusimamia miradi mbalimbali ya kitaifa na kimataifa katika kuwaendeleza watoto, kutokomeza ajira mbaya kwa watoto na kutoa elimu mbadala,kutoa elimu ya ujasiliamali ili kuongeza maarifa katika kujipatia kipato.

Mlote alifafanua kuwa chama kiliona umuhimu mkubwa wa kusomesha mtoto wa kike anayekabiliwa na mazingira magumu kimaisha ambapo jumla ya wasichana 2177, wamepata ufadhili katika ngazi ya elimu ya sekondari na 580 wamefadhiliwa na katika ngazi ya elimu ya msingi.

 Aidha, chama hiki kimesomesha akina mama ..... katika ngazi ya uzamili na uzamivu,ambapo  baadhi ya wasichana waliomaliza sekondari wamefanikiwa kuingia katika vyuo mbalimbali vikiwemo vyuo vikuu.

Mlote anaongeza kuwa zaidi ya watoto 10,125 wameondolewa katika ajira mbaya na kurudishwa shuleni na wengine kupewa elimu mbadala,na lengo letu ni kuwa na mkakati madhubuti na wa makusudi kuongeza idadi ya wanawake katika soko la ajira.

Alisema licha ya juhudi zote hizo katika kumuendeleza mwanamke chama kinakabiliwa na changamoto ambazo ni uwezo mdogo wa chama katika kuwafikia wahitaji na wanachama na kwa kiasi kikubwa chama kinategemea wafadhili katika kutekeleza majukumu yake mbalimbali.

Aidha nyingine ni ugumu wa masharti  kutoka kwa wafadhili wanaotoa misaada na kutokua na ofisi za kudumu za chama katika ngazi za taifa, mikoa na wilaya ili majukumu ya chama hiki yaweze kutekelezwa kama yalivyopangwa.

Aidha aliomba serikali kuwapatiwa ufadhili endelevu kwa kushirikishwa katika mipango ya Serikali inayotakiwa kutekelezwa na sekta binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali katika mpango wa PPP (Public-Private pertnership).

No comments:

Post a Comment