Tuesday, November 27, 2012

MIAKA 50 YA UHURU WA TANZANIA NA MAENDELEO YA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA BARABARA KATIKA MIKOA YA RUKWA NA KATAVI

Nikiianza safari yangu ya kurejea  Bandari salama Dar es salaam kutoka mkoani Katavi ambako nilihudhuria uzinduzi wa mkoa huo, nimepitia barabara ya Mpanda mkoani  Katavi-Sumbawanga mkoani  Rukwa mpaka Tunduma mkoani  Mbeya, ambapo nimejionea mwenyewe na kupata taswira za maeneo  mbalimbali ambayo ujenzi wa barabara ya Tunduma-Sumbawanga-Mpanda unaoendelea kwa kiwango cha lami na kufurahishwa na hatua iliyofikiwa hasa kwa upande wa Sumbawanga -Tunduma.
Ni jambo la kufurahisha kwamba muda mfupi ujao kero ya Usafiri katika mikoa ya Rukwa na Katavi itakuwa ni historia tu, jambo ambalo linafungua fursa mbalimbali za kimaendeleo na kiuchumi katika mikoa hiyo iliyokuwa katika mdororo wa kiuchumi kwa muda mrefu kutokana na miundombinu ya barabara kuwa katika hali mbaya.
Miaka 50 ya uhuru wa Tanzania inaonyesha mwanga wa maendelea katika ukanda huo kutokana na hatua inayopigwa katika ujenzi wa  miundombinu ya barabara, ni wazi kwamba sasa hali ya maisha ya wakazi wa mikoa hiyo itaboreka zaidi kutokana na kufunguka kwa fursa za kimaendeleo kwa wakazi wa mikoa hiyo Asante Serikali kwa kuliona hilo na kulivalia njuga.
Taarifa zaidi ya makampuni yanayojenga barabara hizo, kilomita zake  na gharama ya ujenzi huo utaiona chini ya Taswira hizi endelea kushuka chini mdau.






17.5.1. SEHEMU YA SUMBAWANGA – LAELA (95.31KM)
 Sehemu hii inajegwa na Kampuni ya Aarsleff-BAM International Joint Venture V.O.F Kutoka Denmark na Uholanzi kwa gharama ya dola za Kimarekani 97 Milioni chini ya Mhandisi Mshauri Egis BCEOM International kutoka  Ufarasa.
 Maendeleo ya jumla ya mradi hadi kufikia tarehe 31 Octoba, 2012 yalikuwa yamefikia 49.9% ya kazi zote zilizopangwa.  Kwa ujumla mradi unaendelea vizuri na ulipangwa kwisha 31 Januari 2013 ingawa majadiliano kuhusu kuongeza muda wa kumaliza kazi bado yanaendelea.
 17.5.2. SEHEMU YA LAELA – IKANA (64.2KM)
Sehemu hii inajengwa na Kampuni ya China New Era International Engineering Corporation kutoka China kwa gharama ya Sh. bilioni 76.1 chini ya Mhandisi Mshauri Egis BCEOM International kutoka Ufarasa na unategemea kukamilika 31 Mei 2013.
 Maendeleo ya jumla ya mradi hadi 31 Octoba, 2012 yalikuwa yamefikia 64% ya kazi zote zilizopangwa.  Kwa ujumla mradi unaendelea vizuri.
 17.5.3. SEHEMU YA IKANA – TUNDUMA (63.7KM)
  Sehemu hii inajegwa na Kampuni ya Consolidated Contractors Group S. A (Offshore) (CCC) kutoka Ugiriki chini ya Mhandisi Mshauri Egis BCEOM International kutoka Ufarasa kwa gharama ya Sh. bilioni 82.5.  Maendeleo ya jumla ya mradi hadi sasa yamefikia 43% ya kazi zote zilizopangwa.  Mradi huu ulitegemewa kukamilika tarehe 9 Septemba 2012, hata hivyo  muda wa kumaliza kazi uliongezwa  hadi tarehe 31 May 2013.
 17.6. SUMBAWANGA – NAMANYERE – MPANDA NA KIZI – KIBAONI  (245KM)
 17.6.1. SEHEMU YA SUMBAWANGA – KANAZI (75KM)
 Sehemu hii inajegwa na Kampuni ya Jiangxi Geo-Engineering (Group) Corporation kutoka China chini ya Mhandisi  Mshauri Nicholas O’Dwyer and Company Limited kutoka Ireland akishirikiana na Apex Engineering Ltd.   kutoka Tanzania kwa gharama ya Sh. bilioni  78.8.
 Maendeleo ya jumla ya mradi hadi kufikia tarehe 31 Octoba, 2012 yalikuwa 23.6% ya kazi zote zilizopangwa.  Kasi ya maendeleo ya kazi inasuasua kwa madai kuwa mkandarasi hajalipwa kiasi chote anachodai.   Mradi huu ulitegemewa kukamilika tarehe 15 Desemba, 2012, hata hivyo muda wa kumaliza kazi bado unajadiliwa.
 17.6.2. SEHEMU YA KANAZI – KIZI – KIBAONI (76.6KM)
 Sehemu hii inajegwa na Kampuni ya China Hunan Construction Engineering Group Corporation kutoka China, chini ya Mhandisi Mshauri Nicholas O’Dwyer and Company Limited kutoka Ireland akishirikiana na Apex Engineering Ltd.  kutoka Tanzania, kwa gharama ya Sh. 82.84 bilioni.
 Maendeleo ya jumla ya mradi hadi tarehe 31 Octoba, 2012 yalikuwa 30% ya kazi zote zilizopangwa.  Mkandarasi anaendelea na kazi ingawa kwa kasi ndogo kwa madai ya kuchelewa kulipwa.  Mradi huu ulitegemewa kukamilika tarehe 15 Desemba, 2012, lakini haitawezekana.  Hivyo muda wa kumaliza bado unajadiliwa.
 17.7. SUMBAWANGA – MATAI – KASANGA PORT (112KM)
 Sehemu hii inajegwa na Kampuni ya China Railway 15 Bureau Group Corporation (CR15G)/ Newcentry Company Ltd.  chini ya Mhandisi Mshauri Nicholas O’Dwyer and Company Limited kutoka Ireland akishirikiana na Apex Engineering Ltd,   kutoka Tanzania.  Gharama ya Mradi ni Sh. 133.30 bilioni.
 Maendeleo ya jumla ya mradi hadi kufika tarehe 31 Octoba, 2012 yalikuwa 28% ya kazi zote zilizopangwa.  Mradi huu unatekelezwa kwa mkataba wa Usanifu na Ujenzi (Design and Build Contract).  Kwa sasa kazi zinaendelea vizuri baada ya kusuasua siku za nyuma.  Mradi huu ulitegemewa kukamilika tarehe 13 Januari, 2013 lakini itabidi muda wa utekelezaji kuongezeka kutokana  sababu mbalimbali.

No comments:

Post a Comment