Thursday, November 22, 2012

MWANDISHI MKONGWE AIDAN LIBENANGA AFARIKI DUNIA.


Mke wa mwandishi mkongwe wa habari nchini marehemu, Aidan Libenaga (64), Elizaberth Libenanga (59) katikati akifarijiwa na waombolezaji nyumbani kwake mtaa wa Sabasaba wakati wa kifo cha mume wake aliyefariki dunia hafla majira ya saa 1:00 asubuhi ya leo kwa ugonjwa wa shinikizo la damu (pressure) katika hospitali ya mkoa wa Morogoro mjini hapa.


Na Venance George, Morogoro.
MWANDISHI mwandamizi na ambaye amewahi kufanya kazi katika vyombo mbalimbali vya habari ikiwa ni pamoja na shirika la habari Tanzania (SHIHATA), Aidan Libenanga, amefariki dunia jana.

Kwa mujibu wa mtoto wa marehemu huyo, Ramadhani Libenanga, marehemu alifariki dunia baada ya kufikishwa katika hospitali ya mkoa wa Morogoro majira ya saa 1.00 asubuhi ya jana akiwa anasubuliwa na ugonjwa wa shinikizo la damu (pressure).

Alisema kabla ya kufikwa na umauti huo, mzee Libenanga kama jinsi ambavyo wanahabari wenzake walivyozoea kumwiti aliamka alfajiri majira ya saa 11.30 nyumbani kwake katika kata ya Sabasaba kwa ajili kufua nguo  zake lakini baada ya kuingia bafuni alidodoka chini na kulazimika kukimbizwa hospitali.

“Baba huwa anapenda kufua nguo zake mwenyewe, sasa na asubuhi hiyo aliamka kufua nguo hizo lakini alipoingia bafuni ghafla alidondoka na tukampeleka hospitali ya mkoa kwa matibabu,” alisema Libenanga.

Alisema kuwa cha kusikitisha sana baada ya kufika hospitalini hapo huduma za matibabu kwa baba yake zilichelewa kutokana na kuwepo kwa wagonjwa wa ajali ya barabarani waliofikishwa hospitalini hapo muda huo na hivyo kusababusha mwandishi huyo mkongwe kupoteza maisha akiwa katika harakati za kupatiwa matibabu.

Kuhusu wasifu wake mzee Libenanga alizaliwa katika kijiji cha Libenanga tarafa ya Mwaya, wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro na alipata elimu yake katika shule ya msingi Mwaya kabla ya kujiunga na shule ya sekondari ya wavulana ya Kwiro iliyoko mji wa Mahenge wilayani humo.

Baada ya kuhitimu elimu hiyo, mzee libenanga alichaguliwa kujiunga na sekondari ya Mzumbe kwa kidato cha tano na sita na hatimaye kuajiliwa kama mtumishi wa shirika la posta na simu nchini.

Mwaka 1975, mzee Libenanga alikuwa miongoni mwa waandishi wachache waliochaguwa na chama na serikali kwenda kusomea taaluma ya uandishi wa habari ambapo alikwenda nchini Yugoslavia na kufaulu kwa ngazi astashahada (certificate) na stashahada (diploma) ya uandishi wa habari.

Marehemu aliajiriwa na serikali katika shirika la habari Tanzania kama mkuu wa habari (Bureau chief) katika mikoa mbalimbali ikiwa ni pamoja na Iringa, Kigoma, Shinyanga, Rukwa na Morogoro na baada ya kustaafu kazi alibaki kuwa mwandishi wa kujutegemea akifanya kazi na vyombo mbalimbali vya habari hususan magazeti.

Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya marehemu, Aidan Libenanga, Amina. 

Marehemu ameacha mjane, watoto 10 na wajukuu 10.

No comments:

Post a Comment