Sunday, December 23, 2012

MWAKYEMBE APIGA MARUFUKU VIZUIZI VILIVYOWEKWA NA HALMASHAURI KWENYE BARABARA KUBWA


DAR ES SALAAM, Tanzania

WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amepiga marufuku na kuagiza kuondolewa vizuizi vyote vilivyoanzishwa na Halmashauri kwenye stendi za barabara kubwa kwa ajili ya kukusanya ushuru kwani vinaleta usumbufu kwa abiria.

Kauli hiyo ilitolewa waziri huyo jijini Dar es Salaam, wakati alipofanya ya ziara ya kushtukiza kwenye Kituo cha Mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi majira ya saa 11:30 alfajiri,  ili kujionea utendaji kazi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), na Kikosi cha Usalama Barabarni (Trafic), haswa katika udhibiti wa nauli holela katika kipindi hiki cha sikukuu ya Chrismas na mwaka mpya.

Alisema uwamuzi wake huo unatokana na kubaini kuwa Halmashauri hizo, zimekuwa zikiwalazimisha madereva kuingiza magari (Mabasi), kwenye vituo hivyo ambavyo siyo rasmi  kwa lengo la kujikusanyia  ushuru.

Amevitaja vituo hivyo vilivyolalamikiwa kwa usumbufu huo, kuwa ni pamoja na Mafinga, Kibaigwa, Nzega, Kibaha na vingine.

“Madereva wamekuwa wakilazimishwa kuingia katika stendi hizi hata kama hawana abiria wakushuka amakupakia, kitendo ambacho kinawapotezea abiria muda wao wakufika kule wanakokwenda bila sababu za msingi”alisema Dk Mwakyembe.

Alisema utaratibu huo haukubaliki, endapo ukiachwa uendelee hivyo iko siku watazuka watu watafikia hatua ya kuanzisha vizuizi kama hivyo majumbani mwao lengo likiwa ni kuibia wananchi.

Dk Mwakyembe amezitaka Halmashauri hizo kuacha utaratibu huo na baadala yake watafute vyanzo vingine vya ukusanyaji mapato.

Katika hatua nyingine Dk Mwakyembe amewaonya baadhi polisi wa kikosi cha usalama barabarani kutokana na mtindo wao wakusimamisha magari kwa kushtukiza wakitokea vichakani.

Alisema malalamiko hayo ameyesikia siku nyingi hivyo ameahidi kuwa atayafanyia kazi, ambapo aliwatahadharisha askari wenye tabia kama hizo, watambuwe muda wao sasa unahesabika.

Akizungumzia hali ya usafiri katika kipindi hiki cha sikukuu hizo mbili, Alisema hali aliyoikuta Kituoni hapo inaridhisha kwakuwa abiria wote kwenye mabasi walikuwa wamepata tiketi kwa bei elekezi ya Sumatra.

Dk. Mwakyembe alitoa wito kwa abiria wote kuwa wahakikishe wanatoa ushirikiano kwenye vyombo vinavyohusika pindi watakapotozwa nauli kinyume na ile ya kawaida.

“Msikubali kulipishwa zaidi toeni taarifa haraka, hata katika nauli za mizigo msikubali kulipia mzigo wa kilo 20 atakaekubali yote hayo mtambue amejitakia mwenyewe na asilaumiwe mtu”alisema.

Naye Kaimu Mkurugezi Udhibiti Usafiri wa Barabarani (Sumatra), Leo Ngowi, alisema katika operesheni inayoendelea ya kuyakamata magari yanapandisha nauli holela jana, walifanikiwa kulikamata basi la Kampuni ya KVC lenye usajili namba T709AAT.

Alisema gari hilo lilikwenda kinyume kwa kuwatoza nauli ya sh 35,000 baadala y ash 25,000 abiria waliokuwa wakisafiri kwenda Arusha.

Aidha, Sumatra imetoa leseni za muda kwa wamiliki magagri ambayo yamekidhi viwango vilivyohitajika na mamlaka hiyo, yenye uwezo wa kuchukua abiria 30 kwa lengo la kusaidia kusafirisha abiria wanaofika kwa wingi kituoni hapo ambapo mikoa inayoongoza kwa abiria ni Kilimanjoro, Arusha na Mwanza.

No comments:

Post a Comment