Tuesday, December 18, 2012

SERIKALI MKOANI TABORA YASHINDWA KUSAIDIA MCHEZO WA NETBALL


 Baadhi ya wachezaji wa Netball wakipita kwa maandamano wakitoa heshima katika ufunguzi wa tamasha la kuibua vipaji kupitia mchezo huo kwa mkoa wa Tabora.
 Kabla ya kuingia katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora wachezaji walifanya maandamano na kupita mitaa kadhaa ya mji wa Tabora ikiwa ni sehemu ya hamasa.
Mgeni rasmi katika ufunguzi wa tamasha hilo Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tabora mjini Moshi Abraham maarufu Nkokota akisalimiana na wachezaji.

Uzinduzi wa tamasha la mchezo wa Netball mkoani Tabora umefanyika huku kukiwa hakuna dalili zozote kwa serikali ya mkoa wa Tabora kushiriki kusaidia mchezo huo ambao umetajwa kuwa na lengo kubwa la kuibua vipaji kwa vijana wa kike.


Mwenyekiti wa chama cha Netball manispaa ya Tabora, Zinduna Kambangwa amesema hadi kufikia hatua ya kukamilisha maandalizi ya tamasha hilo wamejitokeza wadau wachache ambao wameweza kusaidia huku akiwataja kuwa ni pamoja na Emmanuel Mwakasaka, Kisamba Tambwe,Mwanne Mchemba na Musoma Batteries.


Hata amekiri pamoja na kupeleka maombi mara kadhaa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Tabora lakini hadi sasa hakuna majibu wala dalili zozote zinazoonesha kusaidia katika kukamilisha tamasha hilo huku hali hiyo ikiendelea kuwatia unyonge wachezaji na wadau wa mpira huo wa pete.


Aidha Zinduna amesema chama chake kitajitahidi kuendelea kutafuta wafadhiri ili waweze kufanya tamasha la aina hiyo kila baada ya miezi mitatu lengo likiwa ni kutafuta namna ya kuibua vipaji kwa wachezaji wa mchezo huo.


Tamasha hilo ambalo limewajumuisha wachezaji wa timu nne za mpira wa pete za hapa manispaa ya Tabora lilianza kwa maandamano yaliyoanzia Shule ya msingi Isike na kupita mitaa kadhaa ya mjini Tabora na kuishia katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi ambapo yalipokelewa na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tabora Moshi Nkokota.   

No comments:

Post a Comment