Tuesday, December 18, 2012

"TUNAMSUBIRI DR.ULIMBOKA ATOE TAARIFA KUHUSU ALIVYOTEKWA"JESHI LA POLISI


DR. STEVEN ULIMBOKA KATIKA PICHA TOFAUTI.
 
 
JESHI la Polisi nchini limesema linamsubiri Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka kufika polisi na kutoa taarifa yake rasmi kuhusu tukio lililomtokea Juni 26, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Mwananchi , msemaji wa jeshi la Polisi Advera Senso amesema wanamsubiri Dk Ulimboka afike polisi na kutoa taarifa yake rasmi pamoja na ushirikiano ili wapate kujua nini kilichotokea.

“Wakati ule hatukumhoji kwa kuwa alikuwa anaumwa tokea hapo, hatujapata taarifa yake hivyo, sisi tunamsubiri aje kutoa taarifa yake na atupe ushirikiano katika suala hilo, tunataka kujua hali yake, lakini sisi tunamsubiri aje ili tupate ushirikiano wake.”

Kabla ya polisi kutoa taarifa hiyo, Oktoba 28, mwaka huu, Dk Ulimboka aliibuka na kusema yuko imara na anajiaanda kuanika waliomteka, kumtesa na kisha kumtupa katika Msitu wa Mabwepande, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Dk Ulimboka alisema kuwa kamwe hajanunuliwa na kuwa kwake kimya kwa muda mrefu kumetokana na kufuatilia kwa karibu masharti ya matibabu yake na si vinginevyo.

“Sijanunuliwa, sijawaogopa watesi wangu, wala sijanyamazishwa kwa lolote lile. Hata hao wanaoeneza taarifa kuwa nimenunuliwa, wanajua kuwa hawana ubavu wa kuninunua. 
 
Bali kimya changu kimetokana na kufuata masharti ya daktari wangu,” ameeleza Dk Ulimboka kujibu swali iwapo kimya chake kimetokana na kununuliwa.

Dk Ulimboka alikiri kuwa amewahi kusikia taarifa za yeye kununuliwa na kwamba huwa anajisikia vibaya anapoona kuna kundi la watu linahaha kutaka kupotosha ukweli na kuchafua jina lake.

“Huo ni uzushi mtupu. 
 
Hata walionitesa wanajua kuwa hawawezi kuninyamazisha au kuninunua. 
 
Wanajua sina bei katika kutetea masilahi ya Umma. Ndiyo maana wakaamua kutumia njia ile ya kinyama kutaka kunitoa roho yangu. Siwaogopi wanaodhuru mwili bali yule awezaye kutoa roho. 
 
Nakuhakikishia, muda si mrefu nitaanika kila kitu juu ya kutekwa kwangu, kuteswa na kutupwa kwenye msitu wa Mabwepande,” ameeleza.

Juni 26, 2012, Dk Ulimboka alitekwa na kuteswa vibaya ambapo alinyofolewa kucha na kutolewa meno na hatimaye kutupwa katika msitu wa Mabwepande.

Mwenyekiti huyo wa Jumuia ya Madaktari Tanzania , aliokolewa asubuhi yake na wasamaria wema karibu na msitu huo, Bunju nje kidogo ya Dar es Salaam.

Akizungumza kwa sauti ya kujiamini, Dk Ulimboka, ambaye bado hajahojiwa na polisi wa Tanzania juu ya aliowataja, amesisitiza kuwa alipokamatwa alikuwa na akili timamu na kwamba waliopanga mkakati wa kumteka anawafahamu.

No comments:

Post a Comment