Sunday, December 30, 2012

taarifa kwa umma:USITISHAJI WA MATANGAZO YA ANALOJIA NA KWENDA KATIKA MFUMO WA DIJITALI

TAARIFA YA MHE. JANUARY Y. MAKAMBA (MB), NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO, SAYANSI NA TEKNOLOJIA KUHUSU USITISHAJI WA MATANGAZO YA ANALOJIA NA KWENDA KATIKA MFUMO WA DIJITALI

Ndugu Wananchi,

Mtakumbuka kuwa hapo tarehe 23 Februari 2012 tuliwatangazia kupitia vyombo vya habari juu ya usitishwaji wa matangazo ya televisheni kwa kutumia teknolojia ya analojia kwenda katika mfumo mpya unaotumia teknolojia ya dijitali.

Napenda kuwaleleza kuwa, maandalizi ya kuzima mitambo ya analojia kuanzia tarehe 31 Desemba 2012 yamekamilika kwa mujibu wa makubaliano ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Hata hivyo, napenda sasa kutoa taarifa kuwa uzimaji wa mitambo ya analojia utafanyika kwa awamu kama ifuatavyo:-

(1) Dar Es Salaam-31 Desemba, 2012;
(2) Dodoma & Tanga- 31 Januari, 2013;
(3) Mwanza-28 Februari, 2013;
(4) Moshi & Arusha-31 Machi, 2013;

(5) Mbeya-30 Aprili, 2013.
Tumeamua kuanza kuzima mitambo hiyo kwa Jiji la Dar es Salaam kwanza ili kutoa fursa kwa makampuni yenye leseni kusimika mitambo ya utangazaji wa dijitali katika mikoa mingine. Makampuni haya yamejipanga kukamilisha usimikaji wa mitambo hiyo katika mikoa minane katika miezi minane ijayo.

Mitambo ya analojia itakayozimwa kesho ni ile iliyopo Kisarawe na Makongo. Vituo ambavyo siku ya tarehe 1 Januari 2013, vitapaswa kuanza kutangaza matangazo kwa mfumo wa dijitali ni TBC1, ITV, EATV, Channel 10, StarTV, DTV, CapitalTV, TumainiTV, ATN, MlimaniTV, C2C, CTN, CloudsTV na Efatha.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inafanya jitihada za kutosha kuhakikisha kwamba makampuni yenye leseni za kusambaza ving’amuzi yanakuwa na ving’amuzi vya kutosha na vingine vimeagizwa ili kukidhi mahitaji ya baadaye na vile vilivyopo sokoni vina ubora unaokubalika.

Vilevile, Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania itahakikisha kwamba zoezi la uhamaji linafanyika bila usumbufu na kero kwa wananchi. Makampuni yanayouza ving’amuzi yameagizwa yaimarishe huduma kwa wateja wakati wa kuuza ving’amuzi na hata baada ya ununuzi iwapo wananchi watakuwa na matatizo na ving’amuzi.

Zoezi hili la uhamaji ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu. Tutakapokuwa tumekamilisha uhamaji, huduma za mawasiliano na utangazaji zitapanuka na kuwa bora zaidi. Kwa mfano, itawezekana sasa kuangalia televisheni kupitia simu zetu za mikononi. Vilevile, itawezekana, kwa bei nafuu kabisa, kwa mtu mwenye uwezo wa kutengeneza vipindi kukodisha chaneli yake na kutangaza vipindi vyake. Vilevile, bei za mawasiliano na utangazaji zitashuka, na tutakuwa tumepiga hatua kubwa kwenye mapinduzi ya teknolojia duniani, ambayo nchi yetu haiwezi kubaki nyuma.

Ndugu Wananchi,

Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu uhamaji huu. Serikali inatarajia kupata ushirikiano wa karibu kutoka kwa wadau wa sekta ya utangazaji na wananchi kwa ujumla katika kipindi cha uzimaji wa mitambo ya utangazaji wa televisheni ili kufanikisha zoezi la uzimaji wa mitambo ya utangazaji ya teknolojia ya analojia.

Uhamaji huu hautahusu televisheni za wananchi zinazopata matangazo kupitia madishi (nyungo) (satellite) au nyaya (cables). Hivyo, wananchi wanaopata matangazo kupitia DStv, Zuku, na nyinginezo wataendelea kupata matangazo yao kama kawaida.

Ndugu Wananchi

Kama kuna mwananchi yoyote ana kero, malalamiko, swali au anahitaji maelekezo kuhusu uhamaji, awasiliane na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kupitia namba 0784-558270; 0784558271 au barua pepe: malalamiko@tcra.go.tz

Ndugu Wananchi,

Nawashukuru kwa kunisikiliza

No comments:

Post a Comment