Tuesday, December 4, 2012

WAKULIMA WA TUMBAKU SIKONGE WAIOMBA SERIKALI


Na Lucas Raphael,Tabora
 
WAKULIMA wa zao la tumbaku kutoka chama cha msingi Ipole wilaya ya Sikonge mkoani Tabora, wametoa kilio chao kwa Serikali kufuatia kucheleweshewa malipo yao baada ya kuuza tumbaku, miezi minne iliyopita.

Wakitoa kilio chao mbele ya mkuu wa mkoa wa Tabora, Fatuma Mwassa wamesema kuwa tangu wauze tumabku hiyo mwezi wa nane mwaka huu, hawajalipwa malipo yao hadi sasa.

Aidha Wakulima hao wamewalaumu viongozi wa chama chao cha msingi Ipole, kwamba wao ndiyo wamekuwa kikwazo kikubwa kulipwa fedha zao kwa wakati.

Wamesema kuwa viongozi wa vyama vya msingi wamekuwa chanzo kikuu cha kuchelewesha malipo ya tumbaku kwa wakulima kwa vile wamekuwa wakiwabambikia madeni ya uongo.

Wakulima hao wa Ipole wamemweleza mkuu huyo wa mkoa wa Tabora kwamba hawaoni umuhimu wa kuwa vyama vya msingi kwa vile vimekuwa haviwasaidii bali ni kuwanyonya, na hivyo kufanya hali ya maisha yao kuwa nyuma kila mara.

Kufautia hali hiyo, wakulima hao wamemuomba mkuu wa Tabora kuingilia kati sakata hilo ili waweze kupata malipo yao haraka iwezekanavyo ili waweze kujikimu.

Wamesema kutokana na kutolipwa fedha hizo wanaishi kwa shida kutokana na kukosa fedha za kununulia mahitaji muhimu ikiwemo chakula na madawa kwa ajili ya kutibiwa wanapougua. 

Hata hivyo Afisa ushirika wilayani Sikonge, Ibrahim Mwarabu na Katibu wa chama cha msingi Ipole Gabriel Kivunde wamesema kuwa kuchelewa kwa malipo hayo kunatokana na baadhi ya wakulima kutorosha tumbaku na kwenda kuuza katika vyma vingine.

Wamesema kwamba wakulima wengi wamekuwa wakitorosha tumbaku zao, kutokana na kuwa na madeni rukuki waliyokopa kwenye chama husika baada ya kukopa pembejeo mbalimbali ikiwemo mboerea na fedha tathilimu. 

Wakati huo huo mbunge wa jimbo la  Sikonge, Said Nkumba amewasa wakulima wa tumbaku mkoani Tabora kuacha kukopa hovyo ili waweze kupata malipo mengi ambapo wakulima wengi  hivi sasa, wanapata fedha kiduchu na wengine kukosa kabisa.

Mwisho


No comments:

Post a Comment