Tuesday, December 18, 2012

SERIKALI YASITISHA UCHIMBAJI DHAHABU SIKONGE


                                        ‘‘ILI KUDHIBITI UCHIMBAJI USIO NA TIJA’’
Na Lucas Raphael, Sikonge

SERIKALI wilayani Sikonge, mkoani Tabora, imepiga marufuku uchimbaji
wa madini ya dhahabu, unaofanywa kiholela na wachimbaji wadogo wadogo
na wakubwa.

Wachimbaji hao wametoka maeneo mbalimbali,mikoa ya Mwanza,Tabora,
Mbeya na Singida, ambao wamevamia maeneo ya machimbo bila kufuata
taratibu za kisheria zinazoongoza rasilimali za nchi kwa manufaa ya
wananchi wa eneo husika na taifa kwa ujumla.

Mkuu wa wilaya ya Sikonge, Hanifa Selengu alitoa amri hiyo jana baada
ya kutembelea machimbo mapya ya dhahabu yaliyoko katika kijiji kipya
cha Kapumpa, kata ya Kitunda, wilayani humo, na kubaini kuwa
wachimbaji wote walioko hapo hakuna hata mmoja aliyefuata sheria na
taratibu zote zinazotakiwa ili kupata kibali cha kuchimba madini hayo.

Akizungumza na viongozi wa serikali ya kijiji, watendaji wa
kata,watendaji wa vitongoji, wadau na wachimbaji wa madini hayo jana,
mkuu huyo wa wilaya, alihoji juu ya taratibu zilizofuatwa mpaka
wachimbaji hao wakaruhusiwa kuanza kuchimba dhahabu hiyo wakati
halmashauri ya wilaya hiyo na ofisi yake, hawana taarifa zozote na
hakuna mtu yeyote aliyeleta barua ya maombi ya uchimbaji katika eneo
hilo.

Selengu alifafanua kuwa eneo lolote lenye madini ama rasilimali,
yanayochimbwa chini ya ardhi mwenye mamlaka kisheria ni rais wa
jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Jakaya Kikwete,ambapo kwa
utaratibu ulivyo wachimbaji walitakiwa waanze michakato ya uchimbaji
ngazi ya halmashauri ya kijiji,na baadaye kamati ya maendeleo ya kata,
WDC,kabla ya kufika wilayani,lakini hayo hayakufuatwa  huku afisa
madini mkazi akitoa kibali bila taratibu zilizopo kisheria kufuatwa.

Wakijibu hoja hiyo watendaji wa kijiji na kata walisema kuwa wao
hawajatoa kibali chochote cha uchimbaji wa dhahabu katika eneo hilo
ila wanachofahamu ni kuwa hawa wachimbaji walikuja na leseni na barua
toka ofisi ya madini mkoani Tabora, na kutuandikia barua ya
utambulisho wa kuja kufanya kazi hiyo ya uchimbaji hapa kijijini.

‘Kwa kweli sisi kama serikali ya kijiji na halmashauri ya kijiji,
hatukuwapa kibali chochote cha kuchimba hayo madini, wao walikuja na
vibali toka mkoani.
Mheshimiwa mkuu wa wilaya…… tunashauri wachimbaji wote wasitishwe
kwanza ili utaratibua ufanyike vizuri kwa manufaa ya serikali ya
kijiji na wilaya yetu’’, alisema afisa mtendaji wa kata ya Kitunda
Julius Ndege.

Wakitoa utetezi wao, wadau na wachimbaji hao walidai kwamba wamefuata
taratibu zote halali na ndio maana serikali ya kijiji imeruhusu
wachimbe madini hayo, japo walikiri kutopeleka maombi yao halmashauri
ya kijiji, ofisi za halmashauri ya wilaya,mkuu wa wilaya hiyo, ili
watambulike rasmi kisheria na ofisi ya mkurugenzi na mkuu wa wilaya
hiyo.

Baada ya kupata maelezo toka pande zote mbili zinazohusika ili
kujiridhisha,mkuu wa wilaya ya Sikonge,Hanifa Selengu, alipongeza nia
njema ya hawa wachimbaji na kubainisha wazi kuwa sheria na taratibu
zimekiukwa, hayumkini hawakujua kuwa ni muhimu kufuata taratibu zote
kuanzia ngazi ya chini ya serikali ya kijiji, kata na hatimaye kupata
kibali toka halmashauri ya wilaya husika.

‘‘Kwa kuwa taratibu zote halali zinazoweza kulinda usalama wenu ninyi
wachimbaji, wanakijiji, serikali ya kijiji na wilaya kwa ujumla
hazikufuatwa, natangaza rasmi kusitisha zoezi zima la uchimbaji wa
dhahabu katika eneo hili la Kapumpa Kitunda Misheni,  mpaka hapo
taratibu zote zinazotakiwa kufuatwa zitakapokamilika’’, alisema mkuu
huyo wa wilaya.

Aidha baada ya tamko hilo,Selengu, aliagiza serikali ya kijiji na
baraza la maendeleo ya kata,WDC, kuanza vikao mara moja na kuweka
utaratibu mzuri ili wananchi wote wajue taratibu zinazotakiwa kufuatwa
kabla ya kuanza kuchimba dhahabu hiyo.

‘‘Kuanzia leo mpaka kesho jioni, wachimbaji wote ondoeni vifaa vyenu
vyote mlivyokuwa mkitumia katika eneo la machimbo, na mchimbaji yeyoye
haruhusiwi kuonekana katika eneo hilo, mpaka awe amefuata taratibu
zote zinazotakiwa kisheria, nashauri mchakato huu ufanyike haraka
iwezekanavyo’’, aliongeza Selengu.

Awali, Mwanasheria wa halmashauri ya wilaya hiyo Richard Unambwe,
akifafanua taratibu na sheria zinazosimamia ardhi na madini hapa
nchini, alisema, kwa mujibu wa kifungu cha sheria ya Ardhi na. 5 (sura
ya 114) ya mwaka 2002, umiliki na udhibiti wa madini yaliyoko ardhini
uko chini ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha Unambwe aliongeza kuwa kifungu Na.6. (1) cha sheria hiyo
kinazuia mtu yeyote kufanya shughuli ya uchimbaji wa madini pasipo
idhini ya mamlaka husika, na kifungu cha sheria ya Ardhi Na.8(1) sura
ya 114 kinaipa mamlaka serikali ya kijiji ya kusimamia ardhi hiyo
kupitia kamati ya ushauri ya halmashauri ya kijiji hicho.

‘‘Ndugu zangu sheria hii ya matumizi ya ardhi, kifungu  Na.8.(6) b
imesisitiza kuwa  matumizi ya ardhi husika yatapitishwa na WDC, pamoja
na hamashauri ya wilaya husika, hivyo ni lazima wilaya ihusishwe
katika suala zima la uchimbaji wa dhahabu na huu ndio utaratibu’’,
alishauri Unambwe.

No comments:

Post a Comment