Sunday, December 23, 2012

SAJUKI AANGUKA JUKWAANI ARUSHA


Msanii wa filamu nchini,Juma Kilowoko akiwa ameshikwa na wasanii wenzake mara baada ya kuanguka jukwaani juzi ndani ya uwanja wa Sheikh Amri katika tamasha la wasanii wa muziki wa kizazi kipya na wale wa filamu.
Msanii wa filamu nchini,Juma Kilowoko akiwa ameshikiliwa na wenzake wakimshusha chini ya jukwaa mara baada ya kuanguka alipopewa nafai ya kuwasalimia mashabiki wake


HALI ya msanii  wa filamu nchini,Juma Said Kilowoko maarufu kama Sajuki imeelezwa si ya kuridhisha  mara baada ya msanii huyo juzi kuanguka jukwaani mara baada ya kuishiwa na nguvu wakati alipopewa kipaza sauti kuwasalimia mashabiki waliofurika kumtizama.

Tukio hilo lilitokea juzi jumapili katika tamasha la wasanii wa filamu na wale wa muziki wa kizazi kipya lililofanyika  ndani ya uwanja wa michezo wa Sheikh Amri Abeid wakati msanii huyo alipopandishwa jukwaani kuwasalimia mashabiki wake.

Mara baada ya msanii huyo kupandishwa jukwaani alipewa kipaza sauti ili aweze kuwasalimia mashabiki wake lakini katika hali ya kawaida alifanikiwa kutamka neno moja tu”ahhh" na kisha kudondoka chini ya jukwaa lakini kabla ya kutua chini alidakwa na wasanii waliokuwa pembeni yake.

Hatahivyo,wasanii hao walimkalisha chini ya jukwaa hilo ili aweze kupumzika na kisha baada ya muda mfupi walimshusha chini ya jukwaaa hilo ili aweze kupata muda wa kupumzika zaidi.

Akihojiwa na gazeti hili muda mfupi mara baada ya kushuka jukwaani Sajuki kwa sauti ya upole alisema kwamba hali yake kiafya si nzuri kwa kuwa hana nguvu na anahitaji matibabu zaidi.

”Kaka hali yangu si nzuri kabisa naumwa sana sijisikii vizuri”alisema Sajuki huku akionekana mnyonge zaidi

Hatahivyo,baadhi ya mashabiki waliokuwa wamefurika uwanjani hapo walionyeshwa kustushwa na hali ya msanii huyo huku wengine wakiwatupia lawama nzito baadhi ya wasanii wa filamu nchini walioambatana na msanii huyo kwa madai kwamba wanamtumia ili wapate pesa ihali mwenzao ni mgonjwa.

Wakihojiwa kwa nyakati tofauti mashabiki hao kwa jazba walisema kwamba msanii huyo alipaswa kupewa muda mwingi wa kupumzika kuliko kuambatana na wenzake mikoani kwani hali hiyo inamchosha zaidi.

“Hawa watu wa Bongo movie ni watu wa ajabu sana huyu mtu anaumwa sana sisi tunashangaa wanaambatana na mtu mgonjwa mikoani wampe muda apumzike na si kumtumia kwa kupata pesa”alisikika shabiki mmoja akiongea kwa jazba
CHANZO: http://woindeshizza.blogspot.com

No comments:

Post a Comment