Sunday, December 23, 2012

WAKULIMA WALALAMIKIA POLISI VIGOGO KULANGUA TUMBAKU - TABORA

Na Mwandishi wetu Tabora.
Baadhi ya wakulima wa zao la tumbaku mkoani Tabora wamelalamikia hatua ya baadhi ya maafisa wa ngazi ya wilaya wa Jeshi la Polisi kujihusisha kununua zao la tumbaku na kubeba kwa kutumia magari ya jeshi hilo.

Wakizungumza wakati wa kutoa hoja mbalimbali zikiwa ni changamoto zinazowakabili wakulima hao katika mkutano mkuu wa 20 wa Chama cha kikuu cha wakulima wa tumbaku kanda ya magharibi mkoani Tabora,moja kati ya vikwazo wamevitaja kuwa ni pamoja na baadhi ya maafisa wa Polisi wilaya ya Sikonge kujihusisha na ununuzi wa zao la tumbaku.

Mmoja kati ya viongozi wa chama cha msingi Ugunda wilayani Sikonge alisema baadhi ya maafisa wa Polisi wilayani humo wamekuwa ni chanzo cha kuchangia utoroshaji wa tumbaku ambayo ilipaswa kuuzwa katika chama hicho na badala yake maafisa hao hununua na tena kwa kuibeba kwa kutumia magari ya Polisi.

Aidha wamethibitisha kuwa kitendo hicho pia kimekuwa kikidumaza nguvu ya vyama vya msingi kwakuwa wakulima wanaowauzia tumbaku maafisa hao wa Polisi mara nyingi wamekuwa wakikwepa kulipa madeni wanayodaiwa na vyama hivyo vya msingi.

Akizungumza katika mkutano huo mkuu wa mkoa wa Tabora Bi.Fatma Mwassa baada ya kupokea malalamiko hayo amesema Serikali ya mkoa wa Tabora haitakubali vitendo vya aina hiyo huku akiwataka viongozi hao wa vyama vya ushirika kuorodhesha majina halisi ya maafisa hao wa Jeshi la Polisi ili waweze kushughulikiwa.

No comments:

Post a Comment