Saturday, December 8, 2012

TANZANIA KUADHIMISHA MIAKA 51 YA UHURU.



Na. Aron Msigwa - MAELEZO.
Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Saidi Meck Sadiki amewaomba wakazi wa jiji la Dar es salaam kujitokeza kwa wingi kuhudhuria sherehe za maadhimisho ya miaka 51 ya Uhuru wa Tanganyika zitakazofanyika katika Uwanja wa Uhuru jiji Dar es salaam.

Maadhimisho hayo yameanzimishishwa mfumo wa aina yake na kuhudhuriwa na viongozi wengi wa ndani na nje ya nchi.

Akitoa ufafanuzi wa kukamilika kwa maandalizi ya sherehe hizo leo jijini Dar es salaam Bw. Saidi Meck Sadiki amesema kuwa maadhimisho ya mwaka huu yatahudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi na mwaka huu mkoa wa Dar es salaam umepewa heshima ya kuandaa sherehe za kutimiza miaka 51 ya uhuru.

Amesema katika kipindi cha miaka 51 ya uhuru Tanzania imepata mafanikio makubwa katika nyanja mbalimbali za uchumi, ulinzi na usalama pamoja na uhusiano wa kimataifa.

Amefafanua kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Jakaya Kikwete na kuongeza kuwa yataongozwa na kauli mbiu isemayo Uwajibikaji, Uadilifu na Uzalendo ni nguzo ya Maendeleo ya Taifa letu.

Aidha amefafanua kuwa sherehe za mwaka huu zitahudhuriwa na ugeni wa marais kutoka Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na kupambwa na gwaride maalum lililoandaliwa na vikosi vya ulinzi na usalama vya Tanzania , halaiki maalum, vikundi mbalimbali vya burudani vya ngoma za asili vya hapa Tanzania hususani kutoka maeneo ya Ukerewe, Dodoma na Zanzibar.

Vikundi vingine vitakavyopamba sherehe hizo ni kundi la Taifa la sanaa kutoka nchini Rwanda (Rwanda National Ballet).

No comments:

Post a Comment