Sunday, December 2, 2012

NJAA YAPIGA HODI VIJIJI VYA NDEVELWA TABORA

Bi.Hadija Mwangatwa mkazi wa kijiji cha Ndevelwa manispaa ya Tabora akijaribu kutayarisha mihogo ili akauze aweze kununua debe la mahindi.

Na mwandishi wetu Tabora.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida tayari imeripotiwa kuwa  vijiji vitatu kata ya Ndevelwa manispaa ya Tabora viko hatarini kukumbwa na njaa hali ambayo imetishia wakazi zaidi ya 6790 waishio kwenye vijiji hivyo.

Wakazi wa vijiji vya kata ya Ndevelwa tayari imebainika kuwa wamekuwa wakila mlo mmoja kwa siku na wengine hata kupitisha siku nzima pasipo kupata chakula. 

Akizungumza na mwandishi wetu  diwani wa kata ya Ndevelwa Bw.Seleman Maganga amekiri kuwepo kwa hali hiyo huku akiitaka serikali kuchukua juhudi za makusudi kukabiliana na janga hilo linalovinyemelea vijiji hivyo.

Diwani huyo Bw.Maganga amesema tatizo hilo ni matokeo ya hali ya ukame iliyovikumba vijiji hivyo tangu mwishoni mwa mwaka jana,na tayari amekwisha lifikisha kwenye vikao vya baraza la madiwani na kujadiliwa.
 
Maganga amefafanua kuwa kwa upande mwingine hali hiyo imechangiwa na idadi kubwa ya vijana waishio vijiji vya Inala,Ituru na Ndevelwa kutoshiriki shughuli za kilimo hata cha bustani  na kuwaachia wazee peke yao ambao huzalisha kidogo kulingana na uwezo wao.  

Aidha alisema idadi kubwa ya vijana wamekuwa wakikimbilia mjini na wale wanaobaki hapo vijijini hujihusisha na vitendo vya kiharifu ilimradi kujihakikishia kipato kisicho cha halali.

Hata hivyo baadhi ya wakazi wa vjijiji hivyo waliolima zao la Muhogo wanalazima kuuza madebe mawili kwa shilingi elfu kumi na sita ili wakanunue debe moja la mahindi ambalo wanadai kuwa ndio linatosheleza kwa mlo wa siku saba katika familia moja.

Mnamo mwaka 2010 oktoba serikali ilitoa chakula cha msaada baada ya vijiji hivyo vya kata ya Ndevelwa kukubwa na mvua kubwa iliyoharibu mazao ya chakula na biashara kama tumbaku na mahindi.

 

 

No comments:

Post a Comment